Skip to main content

Mambo muhimu ya kuzingatia unapohitaji kufanikiwa

Wengi wetu mara nyingi huwa tunafikiri kukosa mafanikio ni matokeo ya kukosa bahati katika maisha. Fikra hizo mara nyingi, huwazuia  wengi katika kufanikiwa na kujikuta wakiishia kuwa  watu wa kulaumu na kushindwa kila siku.

Kimsingi  kitu kikubwa kinachochangia kuzuia mafanikio yetu ni baadhi ya tabia tulizo nazo. Si kweli kwamba watu wengi hushindwa kuendelea kutokana na kukosa mitaji bali ni kwa sababu ya tabia zao. Tabia ni kikwazo kikubwa cha maendeleo ya mtu binafsi kuliko unavyodhani.

Zingatia haya yafuatayo ikiwa unahitaji kufanikiwa katika maisha yako:-

Epuka kufikiria sana juu ya makosa uliyoyafanya.
Kama kuna sehemu ulikosea katika siku za nyuma, hiyo imeshapita chukua hatu za kusonga mbele. Acha kutumia muda wako mwingi na kufikiri pale ulipokosea kwani hiyo haitakusaidia zaidi ya kukurudisha nyuma.

Kumbuka kuwa kukosea ni sehemu ya maisha ya binadamu, kitu cha msingi jifunze kutokana na hayo makosa.

Usiwe mtu wa kuongelea ndoto zako kila siku.
Wengi  wetu tumekuwa ni hodari wa kuzungumza juu ya ndoto zetu, lakini sio watendaji. Kumbuka kuwa kama ni kuongea umeshaongea sana juu ya ndoto zako, umefika sasa wakati wa kutenda.

Jenga tabia ya kuchukua hatua dhidi ya ndoto zako kila siku, hata kama ikiwa ni kwa kidogo kidogo ni lazima utasogea tu, mwisho utajikuta unafanikisha kile unachokitaka.

Usisubiri sana kutekeleza ndoto zako.
Kumbuka hakuna muda sahihi ambao upo wa kuanza kutekeleza ndoto zako kama unavyofikiria. Muda wa mafanikio na kufanya ndoto zako kuwa za kweli ni sasa na wala si kesho. Acha kuwa na tabia au fikra za kufikiri kuwa mipango yako mingi utaifanya siku nyingine. Anza kutekeleza mipango na malengo yako iliyojiwekea mara moja.

Tumia pesa zako vizuri.
Watu wengi huwa ni watumiaji  wabaya wa pesa zao, lakini ni vyema ifahamike kwamba matumizi mabaya ya pesa, ni moja ya tabia kama tabia zingine, lakini ambayo ina nafasi kubwa ya kukukwamisha kwa kiasi kikubwa katika kufikia ndoto na malengo yako uliyojiwekea. Hivyo ili uweze kusonga mbele na kuachana na majuto uliyonayo jifunze kutunza pesa zako vizuri, utafanikiwa.

Epuka kuahirisha ahirisha mambo.
Ikiwa kuna jambo ulipaswa kulifanya leo, basi ni vizuri ukalifanya kuliacha na kutegemea utafanya kesho. Wakati wa kubadilisha maisha yako ni sasa na wala si kesho kama unavyofikiri.

Jiulize ni mara ngapi umesema utafanya kitu fulani kesho na hukufanya? Elewa kwamba tabia hiyo ni mbaya na itakuchelewesha sana kufanikiwa katika maisha.

Anza kujiwekea akiba.
Ikiwa huwa unashindwa kujiwekea akiba katika kipato katika pesa unayoipata basi jua kitakachokutokea katika maisha yako ni kushindwa kumudu kupata pesa ya kuendeshea miradi yako na mwisho wa siku utakuwa ni mtu wa kulalamika tu.

Kama unataka kuwa tajiri na kuwa huru kifedha anza kujifunza kujiwekea akiba, hii itakusaidia sana kusonga mbele katika mambo yako mengi.



Tambua ya kuwa mabadiliko yako yanategemea sana tabia yako ya kimaisha, hivyo anza kujiandaa kubadilika wewe kwanza ikiwa ni pamoja na kubadili hizo tabia ulizonazo ambazo zinakukwamisha sana. Kwa kadiri, utakavyoweza kumudu kubadili tabia zako kwa kiasi kikubwa, ndivyo utakavyo jikuta maisha yako yanakuwa na mafanikio makubwa kuliko unavyofikiri.

Comments

Popular posts from this blog

Wachezaji watatu PSG wakutwa na corona

  Mshambuliaji wa timu ya Paris Saint-Germain,  Neymar de Santos,   ameripotiwa kukutwa na virusi vya corona pamoja na wachezaji wengine watatu. Hata hivyo  Paris Saint-Germain  ambao ni mabingwa watetezi wa Ligi Kuu Ufaransa na kumaliza nafasi ya pili kwenye michuano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya, wameshindwa kuwaweka wazi wachezaji hao wengine ambao wamekutwa na virusi hivyo. Lakini  Angel Di Maria  mwenye umri wa miaka 32 na Leandro Paredes mwenye miaka 26, wanatajwa kuwa kati ya wachezaji hao kwa mujibu wa L’Equipe. Mara baada ya Paris Saint-Germain kumaliza mchezo wa mwisho wa fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya dhidi ya Bayern Munich, Agosti 23, wachezaji hao watatu walionekana kuwa pamoja kwenye visiwa vya Ibiza wakiponda raha ambapo ni Neymar, Di Maria na Paredes.

MWONGOZO WA USAFIRISHAJI WA BIDHAA MUHIMU NA HUDUMA KATIKA NCHI ZA SADC KWA KIPINDI HIKI CHA JANGA LA VIRUSI VYA CORONA

Tarehe 6 Aprili, 2020 ulifanyika Mkutano wa Dharura wa Baraza la Mawaziri wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC).  Mkutano huo ulijadili janga la mlipuko wa ugonjwa wa homa kali ya mapafu (COVID-19) unaosababishwa na virusi vya Corona. Mkutano huo ulihusisha Mawaziri wenye dhamana ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Fedha,Viwanda,Biashara, Utalii, Mambo ya Ndani na Uchukuzi, kutoka nchi 16 wanachama wa SADC ambazo ni Angola, Botswana, Malawi, Mauritius, Msumbiji, Namibia, Jamhuri ya Visiwa vya Ushelisheli, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo na Zambia. Katika mkutano huo, Baraza la Mawaziri lilitoa mwongozo kuhusu Usafirishaji wa Bidhaa Muhimu na Huduma Katika Nchi za SADC katika kipindi hiki cha janga la Virusi vya Corona.  Mwongozo huu utatumika katika kipindi hiki unalenga kupunguza safari zisizo za lazima na usafirishaji wa bidhaa ambazo ni za muhimu tu na unazitaka Nchi Wanachama kuzingatia na kutekeleza sera na miongozo mbalimbali